Afisa TAKUKURU ampiga mwalimu kisa daftari la mahudhurio

0
51

Chama cha Walimu Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kimelaani vikali kiteno cha afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo kumpiga mwalimu wa Shule ya Msingi Kitelewasi akiwa kwenye majukumu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo Mtemi Mgalula amesema kuwa wamefedheheshwa na kitendo hicho na kuwa wameazimia kumpeleka mahakamani afisa.

Mgalula ameongeza kuwa wameazimia kutoshirikiana kwa jambo lolote lile na TAKUKURU Mkoa wa Iringa ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiwazalilisha walimu wawapo kazini.

“Hakuna jambo au tukio lolote ambao walimu wa Wilaya ya Kilolo watashirikiana na TAKUKURU Mkoa wa Iringa hadi pale watakapojirekebisha na kuacha kuwanyanyasa walimu wawapo kazini.”

Akieleza tukio hilo Mwalimu Latifa Kitosi ambaye ndiye aliyeripotiwa kupigwa amesema maafisa hao walifika ofisi na kuomba daftari la mahudhurio ya darasa la sita la mikondo yote miwili lakini kwa haraka daftari la mahudhurio lililokuwepo jirani ni la mkondo B.

Ameema kutoonekana kwa daftari la mkondo A kulibua majibizano baina ya maafisa hao wa TAKUKURU na walimu waliokuwepo katika ofisini, na mmoja ya maafisa hao kumpiga kibao mwalimu na kisha kulichukua daftari hilo la mahudhurio na kumtaka mwalimu huyo kufika katika ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa mahojiano zaidi.

Kitosi amesema maafisa hao walimtuhumu yeye na mwalimu mkuu msaidizi kwa kuharibu ushahidi wa mahudhurio ya mwanafunzi kutokana na kuchelewesha daftari la mahudhurio la mkondo A ambalo ndilo hasa maafisa hao walikuwa wanalihitaji kwa ajili ya kuangalia mahudhurio ya mmoja ya wanafunzi wa darasa hilo.

Amengeza kuwa chanzo cha hayo yote yanatokana na mwanafunzi mmoja kutohudhuria masomo kwa kipindi cha siku kumi na nne bila taarifa yoyote ile kwa uongozi wa shule.

Mwalimu wa Taaluma, Chako Mdemu amesema Novemba 12, 2020 alipata ujumbe mfupi ukieleza kuwa kuna kila dalili za kutoroshwa kwa mwanafunzi huyo kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwa wanafunzi wengine miaka ya nyuma.

Mdemu amesema kuwa baada ya kugundua tatizo hilo ndipo walipotoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ili kuweza kuzuia kutoroshwa kwa mwanafunzi huyo. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mzazi na dada wa mwanafunzi huyo walikiri kuandaa mikakati ya kumtorosha mwanafunzi huyo kinyume na sheria, na ndio kilikuwa chanzo cha dada wa mwanafunzi huyo kupeleka taarifai hiyo TAKUKURU.

Kuhusu ujio wa maafisa hao wa TAKUKURU Mdemu amesema hawakujitambulisha wala kuandikisha kuwa wao ni maafisa TAKUKURU hivyo ili kuwa ngumu kwa viongozi wa serikali ya kijiji na walimu kuwatambua.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Iringa, Domina Mkama amekiri kupigwa kofi kwa mwalimu huyo kutokana na mazingira ambayo walimu hao walikuwa wamemtengenezea afisa huyo hadi kutokea tukio hilo.

Mkama ameema baada ya tukio hilo ndipo daftari la mahudhurio lilitolewa na huyo mwalimu na kuendelea na upelezi.

Ameema serikali kwa serikali hawawezi kugombana hivyo ameuomba uongozi wa Chama cha Walimu Wilaya ya Kilolo kukaa meza moja kuhakikisha wanalimaliza tatizo hilo mara moja ili kuendelea kushirikiana kama ilivyokuwa hapo awali.

Kwa upande wake Katibu wa CWT Wilaya ya Kilolo, Anthony Mang’waru (pichani juu) amesisitiza hawatashirikiana na TAKUKURU mkoani humo hadi pale watakapokaa meza moja na kufikia muafaka na kusitisha vitendo hivyo vya kuwanyanyasa walimu.

Send this to a friend