Afya: Ifahamu dawa kutoka Madagascar inayoripotiwa kutibu corona

0
44

Wakati watafiti na maabara mbalimbali duniani zikiwakatika michakato ya kutafuta dawa ya kutibu homa ya mapafu (COVID-19) inayosababishwa na virusi vya corona, nchi ya Madagascar imetangaza kuwa tayari ina dawa.

Hivi karibuni Rais wa nchi hiyo, Andry Rajoelina alitangaza kuwa wamefanikiwa kupata dawa ya asili yenye uwezo wa kuponya wagonjwa wa COVID-19, taarifa ambayo imeibua mijadala.

“Majaribio yote yamefanyika, na [dawa] ni madhubuti katika kupunguza na kumaliza dalili za COVID-19 kutoka kwa waathrika,” amesema kiongozi huyo akinukuliwa na mtandao wa Africanews.

Baadhi ya wataalamu kutoka nchini Madagascar wameeleza kuwa dawa hiyo inayofahamika kama Covid Organics (CVO), inaimarisha kinga ya mwili na kuua virusi.

CVO inatengenezwa kutoka katika mmea unaofahamika kitaalamu kama ‘Artemesia Annua.’ Asili ya mmea huu ni nchini China na uliingizwa Madagascar kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1970 ili kutibu malaria.

Mmea huo ulipandwa kwa wiki katika Mkoa wa Alaotra Mangoro, lakini uchakataji wake wa viwandani unafanyika katika maeneo ya Itasy, Vakinankaratra, Amoron’i Mania, na Matsiatra Ambony.

Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi za awali zilizoonesha nia ya kuingiza dawa hiyo kwa ajili ya matumizi kwa wananchi wake. Nchi nyingine ambazo zimeonesha nia hiyo, au tayari zimepatiwa CVO ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Guinea Bissau na Senegal.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadhari juu ya matumizi ya dawa binafsi ambazo hazijapitishwa, na kuongeza kuwa haijaidhinisha dawa yoyote itumike kutibu COVID-19.

Wakati onyo hilo likitolewa, raia wa Madagascar wameonekana wakifurika katika meneo zinapogawiwa dawa hizo, ambapo Rais Rajoelina ameagiza zitolewe bure kwa wasio na uwezo, na wenye uwezo wataipata kwa bei chee.

Send this to a friend