Afya: Vyakula vya kuepuka ili upungue na kutokuwa mnene

0
59

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mijadala usiyokuwa na mwisho kuhusu aina ya vyakula mtu anavyotakiwa kutokula mara kwa mara ama kutokula kabisa kama anataka kupunguza unene au anataka asiwe mnene.

Kila mtu kutokana na uelewa wake amekuwa akitaja kile ambacho yeye anakifahamu ambacho alisoma maelezo hayo pahala ama aliambiwa na mwingine.

Katika mjadala huu, watu wengi walionekana kuunga mkono hoja kuwa, ulaji wa vyakula vyenye mafuta ni moja ya sababu inayopelekea watu wengi kunenepa na kuwa na uzito uliopitiliza. Kutokana na Imani hiyo watu wengi wamekuwa wakipunguza kula vyakula vyenye mafuta kama vile nyama, au vyakula vingine vilivyo na mafuta mengi.

Kufuatia mkanganyiko huo, Daktari wa binadamu, Joachim Mabula amekata mzizi wa mgogoro kwa kueleza vyakula vya aina gani huchangia mtu kunenepa zaidi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dr. Mabula ameeleza kuwa vyakula vyenye mafuta si kisababishi kikubwa cha mtu kunene kupita kiasi kama ilivyo kwa vyakula vya wanga, mfano ugali, viazi, wali.

“Ulaji wa vyakula vyenye mafuta haviwezi kukufanya mnene kupita kiasi kama ulaji wa vyakula vya wanga hasa vyenye sukari. Mwili unahitaji mafuta ili kutenda kazi zake vizuri,” ameandika Dr. Mabula.

Aidha, akitoa sababu, amesema kuwa, mafuta yanashughuli nyingi mwilini, hivyo mwili unahitaji mafuta ya kutosha kuweza kufanya kazi kwa ufasaha.

“Mafuta ni muhimu kwa ajili ya kuganda kwa damu unapojikata na misuli kujongea. Mafuta huunda utando wa seli & neva, pia husaidia miili yetu kufyonza vitamini na madini kutoka kwenye vyakula tunavyokula.”

Aidha amesema kuwa, mtu anapoacha kula vyakula vyenye mafuta, hulazimika kula vyakula vya wanga na sukari ambayo kwa pamoja husababisha uzito kuongezeka na kuwa na kiribatumbo.

Dr. Mabula ameongeza kuwa, baadhi ya vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa misuli, mifupa & viungo vya mwili ni pamoja na mayai mfano ya kuku, mboga za majani mfano spinachi, nyama mfano ya ng’ombe, nafaka isiyokobolewa mfano unga wa dona.

Matunda, mboga za majani na mafuta huupa mwili nishati pamoja na vitamini (A, D, E & K) na madini (kalisi/calcium, magnesi/magnesium) ni muhimu kwa misuli iliyojeruhiwa au kuzeeka, aliongeza Dr. Mabula.

Send this to a friend