Agizo la Rais Samia la kushusha bei za mafuta

0
42

Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta hapa nchini zenye thamani ya shilingi bilioni 102 kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta ili kuwapa unafuu wananchi.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Oktoba 5, 2021 wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Utekelezaji wa maagizo hayo umeenda sambamba na marekebisho ya Kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na yatachapishwa katika Gazeti la Serikali leo tarehe 05 Oktoba, 2021.

Rais Samia amechukua hatua hii ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

Aidha, Rais Samia ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni endapo zipo sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta hapa nchini, ili kumlinda mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.