Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete ameitaka Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutazama upya suala la nauli za ndani ili kuwavutia abiria wengi.
Ameyasema hayo mkoani Katavi mara baada ya kutembelea Uwanja wa Ndege wa Mpanda mkoani Katavi ambapo amesema nauli kubwa huchangia uchache wa abiria, ingawa takwimu zinaonesha ongezeko la abiria kwa safari za ndani kupitia kiwanja hicho.
“Takwimu nilizosomewa hapa zinaonesha ongezeko la abiria kwa safari za ndege, naambiwa hapa abiria bado wapo wa kutosha, lakini wanakwazwa na nauli, mkiangalia upya nina imani mtaleta ndege kila siku,” amesema Mwakibete.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusufu ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha ATCL inaongeza safari mkoani humo kutoka safari moja hadi nne kwa wiki, uamuzi uliorahisisha shughuli za kibiashara kati ya mkoa huo na mwingine.