Agizo la serikali malipo ya video vixens & video kings
Serikali imesema walimbwende, wachezaji, waigizaji, wanamitindo na watu wengine ambao hushiriki kwenye Sanaa katika video za wanamuziki kwa lengo la kuiongezea mvuto kazi husika wanafanya kazi kama watu wengine na wanastahili kusimamiwa maslahi na haki zao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum alilouliza juu ya mpango wa kuwatambua na kulinda maslahi ya vijana waliojiajiri katika sanaa ya burudani kama walimbwende.
“Sanaa hii imekuwa ikihitaji ushiriki wa Video Vixen na Video Kings, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria kifungu cha 47(b) mwaka 2019 ili kuipa COSOTA mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mikataba ya kimaslahi kati ya wenye kazi hiyo ya Sanaa na Vijana wetu wa Video Vixen na Video Kings ili waweze kupata haki zao za kimkataba,” amesema Gekul.
Kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999, anayepaswa kulipwa mrabaha wa kazi ya sanaa ni mtunzi, mbunifu na mtayarishaji wa kazi ya Sanaa husika.
Pia, Gekul ametoa rai kwa wadau wote wa Sanaa ya Burudani kuishirikisha Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili maslahi yao yaweze kulindwa kupitia mikataba.