Afisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuchelewa kwa madai ya posho za wachezaji katika michezo kadhaa si sababu ya timu hiyo kutokufanya vizuri hususani katika mechi dhidi ya Azam FC iliyochezwa Mei 07, mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano na E-FM, Ahmed amesema ni jambo la kawaida kwa taasisi kuchelewa kutoa posho kwa wachezaji, na kwamba si mara ya kwanza kwa klabu ya Simba kufungwa na Azam.
“Ni kweli kwamba wachezaji wanadai bonus [posho] zao za mechi kadhaa, na hilo ni jambo la kawaida, kuna wakati taasisi inakuwa na fedha inalipa madeni yote, na kuna wakati taasisi inakuwa haina fedha inalimbikiza madeni, mzigo ukipatikana watu wanalipwa. Na hata wachezaji wa Simba wanafahamu kwamba mzigo ukipatikana kila mmoja analipwa haki yake,” amesema Ahmed.
Ameongeza, katika ‘bonus’ ambayo mtu anadai ni za mechi mbili, mechi tatu, huko nyuma ameshacheza takribani mechi 25 zote amelipwa, tafsiri yake ni kwamba kulipwa kuko pale na ni haki ya mtu kulipwa. Kuchelewa ni masuala ya kawaida kwenye taasisi ya kibiashara.”