Ahukumiwa jela kwa kutumia cheti cha mtu mwingine kujiunga chuo

0
55

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Elina Masawe kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kutumia cheti cha kidato cha nne cha mtu mwingine kujiunga Chuo.

Katika kesi hiyo, Masawe amedaiwa kutumia cheti hicho kusoma kozi ya uuguzi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2012 alipohitimu kozi hiyo ilhali akijua kuwa cheti hicho si chake bali ni cha Sia Ringo.

Akisoma kesi hiyo, Hakimu mkazi mwandamizi, Ramadhani Rugemalira amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa, na upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka hayo kuwa cheti ni acha Sia aliyehitimu kidato cha nne katika shule ya Sekondari Jangwani mwaka 1999.

Fursa za ufadhili wa masomo nchini Israel

Akipitia ushahidi wa upande wa mashtaka, mlalamikaji ameieleza mahakama hiyo kuwa aliwahi kuishi na mshtakiwa kwa lengo la kumlelea watoto wake, pia amewasilisha mahakamani hapo nyaraka muhimu kuthibitisha umiliki halali wa cheti hicho ikiwemo taarifa ya polisi ya upotevu wa cheti na tangazo alilotoa gazetini baada ya kupotelewa na cheti hicho.

Baada ya mahakama kusikiliza utetezi wa mshtakiwa iliamuru mshtakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 5 au kwenda jela miaka mitatu. Baada ya mshtakiwa kushindwa kulipa gharama hizo ilimbidi kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.