Ahukumiwa jela maisha kwa kulawiti watoto, adai alikosa pesa za kuwalipa ‘dada poa’

0
150

Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza imemhukumu kifungo cha maisha jela Isacka Masheku (33), mkulima na mkazi wa kijiji cha Malya, wilayani humo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kulawiti watoto wawili wa kiume wenye umri wa miaka 7 na 9.

Mshtakiwa huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani Julai 23, 2025 na kusomewa mashtaka na wakili wa Serikali, Juma Kiparo katika kesi ya jinai namba 17942/2025, ikielezwa kuwa alitenda makosa hayo mwezi Mei, 2025 katika kijiji cha Malya, wilayani Kwimba kwa nyakati tofauti.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliieleza Mahakama kuwa alikosa fedha za kuwalipa wanawake wanaojiuza kwa ajili ya kumaliza haja zake, hivyo akaona awalawiti watoto hao ambao hawakuhitaji malipo.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na upande wa mashtaka, ambapo wakili Kiparo alisisitiza kuwa kitendo hicho ni cha kikatili na kimewaathiri watoto hao kimwili na kiakili.

Kiparo aliomba Mahakama itumie mamlaka yake kutoa adhabu kali ili kukomesha vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto ambavyo vimeendelea kushamiri katika jamii.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, John Jagadi, amesema Mahakama haina mbadala wa kutoa adhabu nyingine kwani kifungu husika kinatoa adhabu ya kifungo cha maisha pekee, hivyo ameamuru mshtakiwa kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Send this to a friend