Ahukumiwa jela maisha kwa kumbaka mtoto mwenye matatizo ya akili

0
122

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi imemuhukumu Hamisi Rashid Mohamed (55) mkazi wa kijiji cha Mihima Kata ya Namupa Halmashauri ya Mtama Wilaya ya Lindi kifungo cha maisha jela na kumlipa mhanga fidia ya TZS milioni moja kwa kosa la Kubaka mtoto wa miaka 9 ambaye ana matatizo ya afya ya akili.

Imeelezwa kuwa Juni 09, 2024 majira ya saa kumi na mbili jioni, mtuhumiwa huyo alimkuta mhanga njiani na akambeba mgongoni na kwenda naye nyumbani kwake, na kisha kumvua nguo na kumbaka na kumuachia maumivu makali kisha kumtoa nje.

“Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi lilifanya upelelezi mkali kwa kushirikiana na wananchi ndipo mtuhumiwa akakamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa ajili ya kujibu shtaka lake,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Aidha, mahakama imesema hukumu hiyo ni onyo na fundisho kwa watu wenye tabia hizo na inalenga kukomesha kabisa vitendo vya ubakaji na vinavyofanana na hivyo katika jamii.

Send this to a friend