Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mfanyakazi wa ndani

0
84

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemhukumu Suleiman Kwata adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya makusudi dhidi ya Editha Charles, mfanyakazi wa ndani.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, tukio hilo lilitokea Julai 6, 2022, katika eneo la Kimara Temboni, Wilaya ya Ubungo. Mahakama imeeleza kuwa mshtakiwa, ambaye alikuwa jirani wa marehemu, alimuua Editha kwa kumchoma kisu shingoni baada ya kushirikiana naye kuvunja kibubu na kuiba fedha za mwajiri wake kiasi cha shilingi milioni 16.

Imeelezwa kuwa wakati wakiendelea na wizi huo, mshtakiwa alidaiwa kuingiwa na tamaa ya ngono na kutaka kumwingilia kimwili Editha. Alipokataa, alimshambulia kwa nguvu na kumbaka. Tukio hilo lilimkasirisha marehemu, ambaye alimtishia kumfichua kwa mwajiri wake. Hapo ndipo mshtakiwa alipomchoma kisu na kusababisha kifo chake.

Mahakama ilibainisha kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi pamoja na vielelezo uliithibitishia bila shaka kwamba mshtakiwa alihusika moja kwa moja katika mauaji hayo ya kinyama.

Send this to a friend