Ahukumiwa miaka 30 jela kwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha Pili

0
137

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi imemuhukumu kwenda jela miaka 30 Salumu Moshi Mkumbwa (20), mkulima na mkazi wa eneo la Mtanda, Manispaa ya Lindi kwa kosa la kubaka mwanafunzi wa miaka 16 wa kidato cha pili na kumsababishia maambukizi pamoja na maumivu makali.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa kwa nyakati tofauti kuanzia Desemba 2024 hadi Mei 13, 2025, majira ya saa 01:00 usiku, mshitakiwa alikuwa akimlaghai mwanafunzi huyo na kufanya naye mapenzi mpaka pale mama mzazi alipogundua baada ya kumfuatilia kisirisiri.

Mama wa mwanafunzi huyo alimfikisha mwanafunzi huyo Polisi kwa ajili ya msaada zaidi na baada ya Jeshi la Polisi kufanya upelelezi wa kina, lilimkamata mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani kwa ajili ya mashitaka yaliyokuwa yanamkabili, lakini alikana tuhuma hizo. Upande wa Jamhuri ulikuwa na vielelezo vinne na mashahidi watano waliotoa ushahidi wao, ambao ulimtia hatiani mtuhumiwa na mahakama kutoa hukumu ya kwenda jela kifungo cha miaka 30.

Aidha, waendesha mashtaka wamesema hukumu hiyo ni onyo na fundisho kwa watu wenye tabia hizo na itakuwa somo kwa wabakaji wengine au wenye vitendo vinavyofanana na hivyo.

Send this to a friend