Mahakama mkoani Lindi imemhukumu miaka 30 jela mkazi wa Kata ya Ndoro, Manispaa ya Lindi, Naibu Ally (20) baada ya kukutwa na hatia ya kupora simu aina ya Tecno 8 yenye thamani ya shilingi laki sita, mali ya Husna Bilali.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya Mkoa, Conslatta Singano baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Hata hivvyo kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa aliulizwa endapo anazo sababu za msingi ili mahakama impunguzie adhabu, lakini aliendelea kudai kuwa anasingiziwa, na ndipo hakimu alipomuuliza Wakili wa Serikali kama anazo kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa na yeye akajibu kuwa mshtakiwa ni mhalifu sugu na kwamba anazo kesi nyingine katika mahakama ya mwanzo.
Awali wakili wa Serikali aliieleza mahakamani kuwa mshtakiwa akiwa na wenzake wawili, Salum Kambi (24) na Athumani Lwanda (24) ambao wameachiwa huru kutokana na ushahidi kutowatia hatiani, wakiwa na silaha aina ya panga, walimpora mlalamikaji simu hiyo na kutokomea nayo.
Chanzo: Nipashe