Ahukumiwa miaka 50 jela kwa kumkosoa mfalme kupitia Facebook

0
39

Mwanaharakati wa zamani wa demokrasia kutoka nchini Thailand, Mongkol Thirakot (30) amehukumiwa kifungo cha miaka 50 jela kwa kukosoa utawala wa Mfalme Vajiralongkorn na familia yake katika ukurasa wa Facebook.

Hukumu hiyo iliyovunja rekodi imekuja baada ya miaka kadhaa ambapo Thailand imeongeza matumizi ya sheria dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia katika kile wakosoaji wanasema ni mbinu ya kunyamazisha upinzani.

Hapo awali alihukumiwa kifungo cha miaka 28 na mahakama ya chini ya jinai, lakini alipatikana na hatia katika makosa 11 zaidi wakati wa rufaa yake, na kusababisha kifungo cha muda mrefu zaidi.

“Mahakama ya rufaa ilimhukumu Mongkol Thirakot miaka 22 juu ya machapisho yake 27 kwenye Facebook, pamoja na kifungo cha miaka 28 ambacho tayari kimepitishwa na mahakama ya mwanzo. Jumla ya kifungo chake jela ni miaka 50,” Wanasheria wa Haki za Kibinadamu wa Thailand (TLHR) walisema katika taarifa.

Kwa mujibu wa TLHR zaidi ya wanaharakati 250 wameshtakiwa chini ya sheria za udhalilishaji pamoja na sheria kali inayomlinda mfalme na familia yake tangu vuguvugu la maandamano ya 2020 yaanze.

Send this to a friend