Aina mbili za makundi ya watu watakaoondolewa kwenye nyumba za NHC kuanzia Desemba

0
61

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kuanza kuwaondoa wapangaji wa nyumba zake ambao ni wadaiwa sugu kuanzia mapema mwezi Desemba 2021.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaz, Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wapangaji wa shirika hilo jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula NHC inadai takribani bilioni 26 kwa wapangaji wa nyumba zake jambo aliloeleza linachangia kuzorotesha kasi ya utendaji kazi wa shughuli za kila siku za shirika ikiwemo ukarabati

‘’Tutachofanya sasa, yeyote aliyelimbikiza deni na tumeshampa notisi lakini bado halipi kodi basi zoezi la kumwondoa litafanyika bila hata kumtaarifu upya,’’ alisema.

Ameongeza kuwa, oparesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu itaenda sambamba na kuwaondoa wapangaji wote wasio waaminifu waliopangisha nyumba za shirika kwa gharama nafuu huku nao wakipangisha watu wengine kwa gharama kubwa ambapo alikielezea kitendo hicho kuwa ni kuiibia Serikali na halikubaliki kwa kuwa ni kosa kisheria.

Shirika hilo limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake ikiwa ni mpango wa miaka mitano na tayari kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 50 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo

Send this to a friend