Aina tano mpya za upimaji uelewa wa wanafunzi wa elimu ya msingi

0
83

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetoa rasimu ya Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa I – VI ambao umeweka viwango vya utoaji wa elimu kwa kubainisha ujuzi, maarifa, stadi na mwelekeo atakaoujenga mwanafunzi, umahiri wa jumla, maeneo makuu ya ujifunzaji, njia za ufundishaji na ujifunzaji.

Katika mtaala huo umeainisha aina tano za upimaji utakaofanyika kwa wanafunzi katika vipindi mbalimbali vya masomo shuleni;

Upimaji wa awali
Upimaji huu unaelezwa kuwa ni upimaji ambao utafanyika mara tu mwanafunzi anapofika shuleni kabla ya masomo ya darasa la kwanza kuanza ili kupima kiwango cha uelewa na umahiri alionao.

Lengo la upimaji huo ni kumwezesha mwalimu kubaini mahitaji binafsi ya mwanafunzi ili aweze kumsaidia katika ujifunzaji na ufundishaji.

Upimaji gunduzi
Upimaji huu unaelezwa kuwa ni sehemu ya upimaji endelevu ambao utafanyika ili kumwezesha mwalimu kupata taarifa kuhusu uwezo wa mwanafunzi katika kumudu stadi mbalimbali. Taarifa za upimaji zitatumika kutoa ushauri na afua stahiki kwa mwanafunzi mwenye vikwazo katika kujifunza.

Ili upimaji huu uwe fanisi, mtaalamu wa afya anaweza kuhitajika hususani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Upimaji wezeshi
Huu ni upimaji unaofanyika wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji unaendelea kwa kuuliza maswali, mwanafunzi kubaini lengo la ujifunzaji, mwanafunzi kujipima mwenyewe au kupimwa na wanafunzi wenzake. Upimaji huu utamwezesha mwalimu kubaini uelewa na changamoto zinazowakabili wanafunzi wakati mchakato wa ufundishaji

Upimaji endelevu
Kwa mujibu wa TET, upimaji endelevu utahusisha upimaji wa ndani na utafanyika na kuratibiwa shuleni. Mrejesho wa upimaji huu utamwezesha mwalimu kuelewa maeneo yenye changamoto ya ufundishaji na ujifunzaji yanayohitaji kutiliwa mkazo. Upimaji endelevu utachangia asilimia 30 ya upimaji wa mwisho wa Darasa la Sita.

Upimaji tamati
Upimaji tamati utafanyika mwisho wa kila muhula. Upimaji huu utahusisha upimaji wa kitaifa utakaofanyika mwishoni mwa Darasa la Pili, la Nne na la Sita wenye lengo la kubaini kama mwanafunzi amefikia umahiri unaotarajiwa ili avuke darasa moja kwenda lingine.
Aidha, upimaji huu unaelezwa kuwa hautakuwa wa mchujo, bali utatumika kubaini upungufu wa ujifunzaji alionao mwanafunzi ili asaidiwe kabla hajaingia darasa linalofuata.