Akamatwa akitorokea Tanzania baada ya kumkata sehemu za siri mpenzi wake

0
151

Polisi katika Wilaya ya Kyotera Mkoa wa Kati wa Uganda, wanamshikilia Harriet Ampayire mwenye umri wa miaka 23 kwa tuhuma za kumkata sehemu za siri mpenzi wake na kusababisha kifo chake kutokana na kuvuja damu nyingi.

Tukio hilo limetokea usiku wa Jumapili baada ya Ampayire kumtuhumu mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Reagan Karamagi (28) kumsaliti na wanawake wengine.

Ampayire ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya kubeti ya Fort Bet katika mji wa Mutukula, alikamatwa kwenye mpaka wa Mutukula alipokuwa akijaribu kutorokea Tanzania baada ya kutekeleza tukio hilo.

Karamagi ambaye alikuwa dereva wa magari yaliyoagizwa kutoka nje, alikutwa akiwa anavuja damu nyingi usiku wa tukio hilo ambapo licha ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake, alifariki kutokana na majeraha.

Msemaji wa Polisi wa Kanda ya Greater Masaka, Twaha Kasirye amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kwasasa mtuhumiwa yuko chini ya ulinzi katika kituo cha polisi cha Kyotera.

“Walikuwa na ugomvi mdogo usiku wa Jumapili baada ya kurudi kutoka baa ya karibu, na mwanamke huyo alichukua kisu cha jikoni na kukata sehemu za siri za mpenzi wake,” amesema Kasirye.

Kasirye amesema Polisi inafanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka kwa familia ya mwanaume huyo.

Send this to a friend