Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linamshikilia Aurelia Kalolo (40), mkazi wa Kijiji cha Ukumbi, Wilayani Kilolo, kwa tuhuma za kumuua mume wake, Williad Ngamema, kwa kumpiga kichwani na rungu.
Mtendaji wa Kijiji hicho, Mariam Kaduma, alipata taarifa za mauaji hayo siku mbili zilizopita saa tisa usiku na alifika nyumbani kwa wanandoa hao. Alipowakuta, aligundua kuwa mwanaume huyo ameuawa na ndipo alipowataarifu polisi na kumshikilia mtuhumiwa.
Mmoja wa majirani wa karibu na wanandoa hao (jina limehifadhiwa) alisema kuwa ugomvi wa wanandoa hao ulianza tangu asubuhi.
“Jioni, mwanamke alitaka kumpiga mume wake na rungu, tukasuluhisha. Baadaye, akaondoka na kwenda kilabuni kunywa pombe. Kumbe usiku aliporudi, alichukua tena rungu na kumpiga mume wake, ambaye amefariki,” alisema.
Matumizi ya bangi Kenya yaongezeka mara dufu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi la polisi linaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo.
Naye Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga, alisema chuki, hasira, na visasi ndani ya ndoa vimekuwa vichocheo vya ukatili na mauaji kwenye familia. Alipendekeza kuwashirikisha wazee na viongozi wa dini kutatua migogoro ya familia na kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Chanzo: Mwananchi