Akamatwa na kobe 998, adai ni tiba ya UKIMWI

0
41

Mwanaume mmoja mkazi wa Kijiji cha Nyarukoru, mkoani Mara, Matimba Washa (28), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Butiama kwa makosa matatu likiwemo kukutwa na kobe 998, magamba 10 ya kobe, ngozi ya Nyati na mkia wa Nyumbu, vyenye jumla ya thamani ya TZS milioni 168.

Katika mahojiano yake na Polisi mshitakiwa amedai kuwa ameoteshwa na mapepo kuwa nyara hizo za Serikali ni tiba ya magonjwa kama vile UKIMWI, Selimundu na magonjwa mengine ya zinaa hivyo kuwaomba wamletee mtu yeyote mahakamani hapo mwenye ugonjwa mmojawapo ili awathibitishie uwezo wa dawa hizo.

Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Gaston Kayombo amesema mshitakiwa huyo anashitakiwa kwa makosa matatu ya kukutwa na nyara za serikali pamoja na uhujumu uchumi.

“Mashitaka haya yapo mahakamani hapa chini ya kifungu cha 86 kifungu kidogo cha 1 na cha 2(c), 3(c) ya Sheria ya Wanyamapori, Sura ya 283 marejeo ya 2022 ikisomwa na aya ya 14 ya jedwali la kwanza la kifungu cha 57 na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 ya mwaka 2022,” amesema Kayombo.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend