Akaunti 25 za ku-follow Twitter Tanzania (ToT) mwaka 2021

0
21

Mwaka 2020 unaelekea mwisho, na huku maandalizi ya mwaka mpya, 2021, yakiendelea. Leo nakusogezea mchongo wa akaunti 25 za mtandao wa Twitter kutoka Tanzania ambazo ukizifuata (follow) utaweza kufahamu masuala mbalimbali kuanzia burudani, siasa, uchumi, vyakula na ubashani usio na faida.

Mpangilio wa orodha hii haujafuata mfumo wa umuhimu.

Maria Sarungi
Tweets zake nyingi ni masuala ya kiasiasa na uchumi. Unataka kujua Trump kasemaje, au nini kinaendelea kwenye siasa za Tanzania, basi hii itakufaa.

MasoudKipanya
Jamaa ana akili sana, hii inajiridhisha kupitia kazi yake ya uchoraji katuni ambazo nyingi hubeba jumbe za kisiasa. Fanya kumfuata uumize akili kung’amua anachomaanisha.

Abbymexahnk
Mbali na kuwa anaabudu chapati, ila akiamua kuwa serious huwa anatweet masuala ya kazi ambayo huwa ni msaada kwa wengi. Kupitia kwake utajua mambo ya kuzingatia kwenye interviews, barua ya maombi ya kazi inaandikwaje, nini cha kufanya na cha kutofanya ukiwa kazini.

Fatma Karume
Wanapenda kumuita shangazi. Kutoka katika familia ya kisiasa kwenye visiwa vya Marashi ya karafuu, utapata kufahamu masuala ya kisiasa na harakati za kidemokrasia. Kikubwa, angalia Kiingereza chake kisiku-suffocate.

Marekamalili
Baba Magie anapenda bia, lakini akiwa hajanywa huandika tweets zenye akili kuhusu maisha ya kila siku, huku akishauri watu vitu vya kufanya, mambo ya kuzingatia kuweza kufanikiwa.

Chapo255
Kwa lugha ya kimombo wanamuita Content Creator. Huyu ana kazi moja tu, kufunua kapeti ujue zile za kiburudani ambazo pengine huwezi kuzipata popote.

Michaelmwebe
Masuala ya michezo, Mapokezi FC ni nani, timu gani inategemea mchezaji mmoja, nani atamfunga nani, yote yanajibiwa kwenye akaunti hii.

Blizzss
Jamaa anapenda movies, lakini hiyo siyo sababu iliyomfanya awepo hapa, japo siyo mbaya ikijua hilo. Huwa hana shughuli ndogo inapokuja kwenye chakula kizuri. Ukitaka kujua wapi kuna biridani, kuku wa kupaka, sotojo la jioni, we tafuta bando, majibu anayo.

Ellipsis Digital
Teknolojia inazidi kushika kasi nchini Tanzania, na vijana wengi wameonesha utayari wa kuwekeza kutumia fursa hiyo. Hii ni moja ya kampuni za kidijitali za vijana wa Tanzania zinazotoa huduma za software kwa kampuni changa, biashara na mashirika duniani kote.

Danny Msirikale
Unataka kusafiri Tanzania ukiwa umekaa ndani kwako? Hapa shughuli ni moja, picha zenye viwango vya SGR. Ukitaka picha za kuweka ofisini, nyumbani au popote, mcheki. Mikono yake imebarikiwa.

Adeck Juice
Hapa analiwakilisha kundi la wajasiriamali wa Twitter. Kwake utapata sharubati za maana sana, ukiagiza, inakuja kama ulivyoiona kwenye picha.

TOTBonanza
Mara tatu kwa mwaka, Watanzania waliopo Twitter hujumuika pamoja na kufurahia maisha. Hii ndiyo akaunti inayoratibu shughuli zote. Ukiifuata, utaweza kujua lini watu wanakutana wapi, na kutakuwa zipi.

Adambrv
Zile Life Hacks utazipata hapa. Anakuletea taarifa za nyumba bora iweje, hujakaa vizuri anakupa wazo la biashara na kama unayo tayari, basi atapata wazo la namna ya kuiboresha. Yeye anamwaga mchele, anawaachia kuku wale wawezavyo.

Bookmartz
Unapenda kusoma vitabu? Basi kiu yako ya kutafuta sehemu ya kuvipata imeishia hapa.

MuroKing
Yeye anajiita Lomayani. Stori za muziki wa Tanzania, hasa Hip Hop, mafaili anayo yeye. Ukimnunulia juisi akiwa ufukweni atakueleza mambo ya muziki ambayo huyajui.

Gillsaint
Hili ni darasa lisilo na mwenyewe. Vijana wengi wanajifunza kwake namna anavyojituma, na pia huwasaidia vijana wengi kuweza kujikwamua kimaisha

KennedyMmari
Kutoka kwake utapata taarifa mbalimbali zinazohusu vijana, siasa mara moja moja na masuala ya kijamii

BarakaSaimon3
Ukitaka kutoka na mguuni pawe pamekaa sawa, basi hapa umefika. Baraka ni mmoja wa wajasiriamali wengi wanaofanya biashara kupitia mtandao wa Twitter.

Tanpol
Ukurasa wa Jeshi la Polisi Tanzania hutoa taarifa mbalimbali kuhusu ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Udadisi
Jina la akaunti linasadifu maudhui. Mwanazuoni Mwafrika anayependa majadiliano hasa masuala ya siasa na uchumi. Sifa nyingine ni matumizi ya kiswahili, huenda ukahitaji kamusi ya Kiswahili ukipitia ukurasa wake.

Tonytogolani
Wakati mwingine anachoandika unajiuliza alikuwa anawaza nini, au wewe mbona hukuwahi kukiwaza wakati kinaonekana wazi. Amekuwa akitoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali juu ya namna ya kuendesha maisha ya kila siku. Ila vijana wengi wanampenda mshauri wake wa masuala ya burudani na anasa.

MenThePodcast
Hapa utapata mijadala inayohusu afya ya akili kwa wanaume. Ni moja ya akaunti ambazo zinasaidia kukabiliana na changamoto za afya ya akili kwa kujadili masuala ya kiakili yanayowakabili wanaume.

YourFrenchFry
Maisha hayapo serious sana, wakati mwingine unahitaji umbea kidogo ujue huyu ana crush kwa nani, huyu amemfanyaje mpenzi wake, nani alichomeshwa mahindi stendi, ili mradi maisha yaende. Coco anakukisanyia zote na kuzileta TL.

World Bank Tanzania
Ukurasa huu utakujuza habari mbalimbali kuhusu maendeleo ya uchumi wa Tanzania na shughuli za kibiashara zinazofanyika nchini.

ElimikaWikiendi
Kila wikiendi tunakusanyika kwenye jamvi hili linalolenga kukuza lugha ya Kiswahili kujadili masuala yatakayotuelimisha. Kupitia watoaji mada utaweza kujua mambo mbalimbali, ya kiafya, historia n.k.

Hizi ni baadhi tu ya kurasa mbalimbali kwenye matandao wa Twitter unazoweza kuzifuata kupata habari mchanganyiko. Si vibaya pia ukitufuata Swahili Times uweze kupata habari mbalimbali saa 24.

Send this to a friend