Akiri kumbaka mtoto wa miaka mitano, adai ni shetani alimpitia

0
2

Mahakama ya wilaya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu Nicholaus Paulo Kidoganya (21) mkazi wa Kijiji cha Nyehunge, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitano.

Mwendesha Mashtaka ameieleza Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 23, 2024, katika Kijiji cha Nyamadoke, wilaya ya Sengerema, mkoa humo kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(a) pamoja na kifungu cha 131(3) cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema baada ya kufikishwa mahakamani na kusomewa shtaka hilo, kwa hiari yake bila kuisumbua mahakama mshtakiwa aliamua kukiri kutenda kosa la kumbaka mtoto huyo ambapo ameeleza kuwa siku ya tukio alimshawishi mtoto huyo kwa kumhahidi kumpa maembe yaliyokuwa juu ya mti wa maembe uliokuwa kwenye shamba la mahindi.

“Baada ya mhanga kufika eneo hilo alimkamata na kumuingilia kimwili mpaka alipokutwa na kukamatwa na mwalimu wa shule ya msingi Nyamadoke iliyo karibu na eneo hilo (jina la mwalimu limehifadhiwa) akiwa anafanya kitendo hicho cha ubakaji.

Baada ya Mahakama kupitia vifungu vya sheria na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ikiwemo ripoti ya Mganga aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, pamoja na cheti cha kuzaliwa cha mhanga, Mahakama imejiridhisha bila ya kuacha shaka kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo licha ya ukiri wake.” Imeeleza.

Aidha, baada ya kutiwa hatiani mshtakiwa aliiomba Mahakama imuachilie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kudai kuwa alipitiwa na shetani.

Send this to a friend