Aliyeambiwa ana saratani na kutolewa tezi kimakosa azidai hospitali milioni 500

0
23

Florence Samwel ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Kilimo amezishtaki Hospitali za TMJ na Hindu Mandal pamoja na Dkt. Maurice Mavura katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya uchunguzi aliofanyiwa katika Hospitali ya Apollo nchini India kutoa majibu tofauti na aliyopewa nchini.

Mlalamikaji  huyo anadai fidia ya TZS milioni 500 kwa madhara aliyoyapata kutokana na makosa aliyofanyiwa na hospitali hizo ambapo anadai kuelezwa kuwa ana saratani na hata kuondolewa tezi moja, hivyo kulazimika kuishi kwa kutumia dawa maisha yake yote ilhali hana tatizo hilo.

Aidha, ametaka alipwe TZS milioni 53 za gharama za dawa anazotumia kutokana na makosa yaliyofanyika pamoja na gharama za usafiri alizokwenda kutibiwa nchini India ambapo alifanyiwa uchunguzi na kubainika hakuwa na saratani kama alivyoelezwa awali.

Ameongeza kuwa uchunguzi kutoka Hospitali ya Apollo nchini humo uligundua kuwa ameondolewa tezi ya kushoto jambo ambalo hakuelezwa na Dkt. Mavura ambaye alielekezwa kwake na hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakati alipokwenda kufanya uchunguzi wa koo.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend