Mchoraji, Shadrack Chaula (24) aliyehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni ameachiwa huru baada ya kulipa faini ya shilingi milioni tano.
Chaula ambaye alikamatwa Julai 04, mwaka huu baada ya kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na kushtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo mitandaoni, alihukumiwa adhabu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya mara baada ya kushindwa kulipa faini.
Hata hivyo akiwa jela, baadhi ya watumiaji wa mtandao wa X (zamani Twitter) akiwemo Wakili Peter Kibatala walianza michango mtandaoni ili kutimiza kiasi cha faini kinachohitajika.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Wakili Kibatala amethibitisha kuwa kijana huyo yuko huru, huku wakiwa katika picha ya pamoja akiambatanisha na ujumbe wa shukrani kwa wote walioshiriki kuchanga fedha hizo.