
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART) kumlipa Frank Zebaza fidia ya shilingi milioni 88.8, baada ya kugongwa na basi la Mwendokasi.
Katika hukumu iliyotolewa Desemba 19, 2025, mahakama pia imebaini kuwa dereva wa basi hilo, Hafidhi Ally, alikuwa akiendesha kwa uzembe na akamwamuru kumlipa mlalamikaji shilingi milioni 10 binafsi.
Uamuzi huo umetokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Zebaza dhidi ya UDART, dereva wa basi, Shirika la Bima la Taifa (NIC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Awali, Zebaza alikuwa akiomba fidia ya jumla ya TZS milioni 600 kwa majeraha aliyoyapata katika ajali hiyo.
Katika madai yake, alidai TZS milioni 350 kama fidia maalum kwa gharama za matibabu na matumizi mengine yanayohusiana, TZS milioni 150 kama fidia ya jumla kwa maumivu na mateso, pamoja na TZS milioni 100 kama fidia ya adhabu.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Griffin Mwakapeje amesema ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonesha wazi kuwa mlalamikaji alipata majeraha makubwa yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji mkubwa na hadi sasa anaendelea kukumbwa na athari za kudumu katika mfumo wa fahamu na hisia, hali iliyosababisha kupungua kwa uwezo wake wa kufanya kazi.
Ajali hiyo ilitokea Septemba 30, 2022, wakati Zebaza alipokuwa akitembea kando ya Barabara ya Morogoro, eneo la Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo aligongwa na basi la mwendokasi aina ya Golden Dragon lenye namba ya usajili T132 DGW.








