Aliyeiba bia za mama yake ajinyonga rumande baada ya mama yake kukataa kumfutia kesi

0
4

Polisi katika mji wa Eldoret nchini Kenya wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha Collins Cheruiyot, kijana mwenye umri wa miaka 24, aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kuvunja na kuingia katika baa ya mama yake na kuiba pombe, kufariki dunia kwa kujinyonga akiwa rumande.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Turbo, Patrick Wekesa, marehemu aliamua kujitoa uhai baada ya juhudi zake za kumshawishi mama yake kufuta kesi dhidi yake kugonga mwamba. Inasemekana kuwa kabla ya tukio hilo, Cheruiyot alimwomba mama yake msamaha na kumsihi afike mahakamani ili kusuluhisha suala hilo nje ya mahakama, lakini mama yake alikataa ombi hilo.

Cheruiyot alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Mei 27, 2024, ambapo alikiri shtaka la wizi lakini baadaye alibadili msimamo wake na kuomba kupewa nafasi ya kujitetea. Hata hivyo, kesi yake iliendelea kuahirishwa huku akiomba mahakama impe muda wa kumshawishi mama yake aiondoe.

Baada ya kurejeshwa rumande, Februari 12, 2025, Cheruiyot alimpigia simu ya mwisho mama yake akimsihi afike mahakamani kumwokoa, lakini juhudi zake hazikufua dafu. Kwa huzuni na kukata tamaa alijinyonga ndani ya chumba cha mahabusu.

Polisi wanasema maafisa wa mahakama na wafungwa wengine walijaribu kumuokoa lakini walichelewa, na alitangazwa kuwa amefariki alipofikishwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) mjini Eldoret.

Send this to a friend