Aliyekuwa bosi wa Bohari ya Dawa ashtakiwa kwa utakatishaji wa bilioni 1.6

0
15

Waliokuwa vigogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini Tanzania leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matano yanayowakabili katika Namba 46 ya mwaka 2020.

Watuhumiwa hao waliofikishwa mahamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurien Bwanakunu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Byekwaso Tabura.

Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah amesema kuwa wawili hao walitenda makosa yote kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019.

Akisoma mashtaka hayo amesema kuwa shtaka la kwanza linawahusu wote wawili ambapo wanatuhumiwa kupanga njama na kutenda kosa kinyume na kifungu Namba 200 cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002.

Katika shtaka la pili watuhumiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya TZS 3.8 bilioni.

Shitaka la tatu la matumizi mabaya ya madaraka linamhusu Bwanakunu ambapo inadaiwa kuwa aliongeza mishahara na posho kiasi cha shilingi bilioni 3.8 kwa watumishi wa mamlaka hiyo bila idhini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma.

Kosa la nne linawahusu watuhumiwa wote wawili ambapo na kwamba wameisababishia Bohari ya Dawa hasara ya shilingi milioni 85 baada ya kufanya uzembe na kutokea uharibifu wa dawa zilizokuwa zimehifadhiwa katika bohari hiyo.

Shtaka la mwisho ni utakatishaji wa TZS 1.6 bilioni ambapo watuhumiwa wote wawili wanatuhumiwa kulitenda kinyume na Sheria Namba 12 ya mwaka 2006 ya Utakatishaji wa Fedha na kifungu namba 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002.

Hakimu Kabate ameiahirisha kesi hiyo mpaka Juni 19, 2020, itakaporeje tena kwa ajili ya kutajwa.

Send this to a friend