Aliyekuwa DC Tabora Mjini kufungua shauri kupinga uamuzi wa Rais Samia kumstaafisha

0
35

Mahakama Kuu Masijala Kuu imemruhusu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Komanya Kitwala kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kumlazimisha kustaafu kabla ya muda wake.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Lilian Mongela Mei 23, 2023 katika shauri la maombi lililofunguliwa na Kitwala dhidi ya Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Jaji Mongela amemtaka kufungua shauri hilo ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kurejea sheria na uamuzi wa kesi mbalimbali za mahakama hiyo na Mahakama ya Rufani, amekubaliana na hoja za wakili wa Kitwala, Jeremiah Mtobesya kwamba mwombaji amekidhi vigezo kustahiki kupewa ruhusa hiyo.

Kitwala aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuhakiki mali za Chama cha Mapinduzi (CCM) aliteuliwa Julai 27, 2018 na Hayati Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini ambapo kabla ya uteuzi huo, alikuwa akifanya kazi PSSSF kama Ofisa Sheria.

Uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia Juni 19, 2021 na nafasi yake kuchukuliwa na Dkt. Yahya Nawanda, na ndipo alimwandikia barua Katibu Mkuu Utumishi, akiomba kurejeshwa katika ajira yake ya awali (PSSF) ambayo amedai haikujibiwa mapema mpaka alipopokea barua ya Katibu Mkuu Kiongozi Agosti 15, 2022 iliyomfahamisha kuwa Rais amemstaafisha kwa maslahi ya umma.

Kitwala anataka kuiomba Mahakama iitishe, kisha kutengua na kutupilia mbali uamuzi wa Rais kwa kudai amekwenda nje ya mamlaka yake kisheria dhidi ya kanuni ya haki asili, pia Katibu Mkuu, Utumishi amrudishe katika ajira yake ya awali kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wa Wilaya na kulipwa madeni ya mishahara na mafao kuanzia Juni 28, 2021 mpaka tarehe ya kurejeshwa katika ajira yake.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend