Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ameng’oa miundombinu ya maji aliyokuwa ameiwezesha kufungwa wakati akitumikia wadhifa huo, hatua aliyochukua siku chache baada ya kung’olewa kutokana na tuhuma mbalimbali.
Taarifa ya gazeti la Raia Mwema inaeleza kwamba juzi alikwenda katika Uwanja wa Mandela ulioko Pasua na kung’oa miundombinu ya maji aliyoitoa siku za nyuma kwa vijana wanaotumia uwanja huo.
Mkazi wa Pasua, Waziri Shemanguzo amesema kwamba kitendo alichokifanya si cha kiuungwana kwani hata kama ametolewa, kwenda kuondoa misaada aliyoipatia jamii sio jambo la kiuungwana.
“Ni kweli nilitoa msaada wa kuwavutia maji kwenye Uwanja wa Mandela, lakini maji hayo yalikuwa yakiacha tu na kumwagika muda wote, maana palikosa usimamizi, hivyo ikawa inaletwa bili kubwa,” amesema Raibu.
Raibu alitolewa kwenye nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na hayo ilidaiwa kushiriki sherehe ya kijana anayedaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, pia kuhamisha fedha kutoka Kituo cha Afya Kaloleni na kuzipeleka Kata ya Pasua bila kufuata utaratibu, vitendo vya rushwa, ujenzi holela katikati ya mji na kuwakashifu madiwani wenzake.