Aliyemuua mke wake kisa sadaka auawa

0
44

Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Bernard Odweso mwenye umri wa miaka 60 ameuawa na wananchi baada ya kudaiwa kumchoma mkewe kisu hadi kufa katika kijiji cha Nyalula, Kaunti ya Siaya nchini Kenya, chanzo kikidaiwa kuwa ni pesa ya sadaka.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Siaya, Cleti Kimaiyo amesema mwanaume huyo anadaiwa kumshambulia Pamela Anyango (55) siku ya Jumapili baada ya ugomvi juu ya KSH 30 [TZS 640] zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sadaka kanisani, ambazo mwanaume huyo alishutumiwa kuwa amezichukua.

Ameeleza kuwa baada ya kuulizwa kuhusu pesa hizo za sadaka, Odweso alikuwa mkali na ndipo alipomshambulia mke wake kwa kumchoma kisu mara kadhaa na kufariki papo hapo huku binti yake mwenye umri wa miaka 22 akifanikiwa kukimbia.

Mwanaume huyo hakuishia hapo, alianza kumshambulia mtoto wake wa kiume kwa kumchoma kisu kwenye shingo na mguu wa kushoto alipojaribu kumtuliza.

Kamanda wa polisi ameeleza kuwa baada ya kupata habari za tukio hilo, wanakijiji na majirani walimzonga Odweso na kumshambulia kwa kumpiga vibaya kichwani, na alipokimbizwa hospitalini akiwa na hali mbaya, alipoteza maisha.

Send this to a friend