Aliyevaa sare za JWTZ ili asikataliwe na mchumba wake ahukumiwa kwenda jela

0
14

Mahakama ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemuhukumu kifungo cha miezi sita Rajabu Reli (22), mkazi wa Sengerema baada ya kukutwa na hatia ya kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bila ruhusa.

Hukumu hiyo imetolewa jana tarehe 07.01.2025 katika shauri la jinai namba 445 la mwaka 2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Mhe. Evodius Kisoka mbele ya mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro mbele ya hakimu Evodius Kisoka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 5, 2024 kijiji cha Kasisa, wilaya ya Sengerema na kufikishwa mahakamani januari 07, 2025.

Baada ya kusikiliza pande zote za ushahidi hakimu Evodius Kisoka alijiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni mzito na haukuacha shaka lolote.

Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetetea kwanini asipewe adhabu; aliomba mahakama hiyo imuachie huru kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na alivaa ili akubaliwe na mchumba wake.

Hata hivyo, ombi hilo lilitupiliwa mbali na Hakimu Kisoka na kutoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya Rajabu.