Aliyewazalisha wanawake wawili kwenye geti la zahanati ajengewa nyumba

0
87

Wananchi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamechukua jukumu la kumjengea nyumba mkunga wa jadi kama shukrani baada ya mkunga huyo kuwazalisha wanawake wawili katika geti la zahanati ya Kashai.

Inadaiwa kuwa, mkunga huyo alifanya hivyo mara baada ya wanawake hao kutofunguliwa na wahudumu wa zahanati hiyo huku wakiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua, ndipo alipoamua kuwazalisha na kuwaokoa akina mama hao na watoto wao wawili.

Mara baada ya tukio hilo wananchi walianzisha kampeni ya kumjengea nyumba ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 iliyochukua takribani siku 23 mpaka kukamilika.

Aidha, Diwani wa Kata ya Kashai, Ramadhani Kambuga ameishukuru TANESCO kwa kufikisha huduma ya umeme bila malipo yoyote katika nyumba ya mkunga huyo pamoja na wananchi wote waliochangia ujenzi huo.