Aliyosema Rais kuhusu vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro.
Ajali hiyo imetokea leo tarehe 10 Agosti, 2019 majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.
Rais Magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii na pia amewaombea majeruhi wapone haraka.
“Nimeumia sana kusikia idadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za Marehemu wote, nawaombea Marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka” amesema Rais Magufuli na kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na vifo hivyo.
Rais Magufuli ameagiza Wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na ametaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa Maisha yao.
Aidha, Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbalimbali zilizobebwa na magari hayo na ametaka vitendo hivyo vikome.
“Baadhi ya magari haya yanabeba mafuta ambayo ni hatari kama ilivyotokea Morogoro, yapo magari yanabeba kemikali za sumu, yapo magari yanabeba milipuko nakadhalika, nawaomba sana tuache tabia hii” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.