Amchoma mkewe kisu nyumbani kwao baada ya kumkimbia na watoto
Polisi katika kijiji cha Kibaita, Kaunti ya Nandi nchini Nairobi, wanachunguza tukio la kusikitisha ambapo mwanaume aliyefahamika kwa jina la Hanise Juma amemchoma kisu mkewe, Winnie Akusuha hadi kufa kabla ya kujiua.
Kamanda wa Polisi wa Nandi Kusini, Maina Nduriri amesema tukio hilo limetokea Jumatano usiku baada ya ugomvi wa kimapenzi kati ya wanandoa hao.
Imeelezwa kuwa mwanaume huyo alimfuata mkewe hadi Narok baada ya mkewe kuondoka nyumbani pamoja na watoto wao watatu kufuatia kutokuelewana, na Juma aliingia nyumbani kwao kwa siri majira ya saa moja na kumvamia Winnie, aliyekuwa jikoni akipika chakula cha jioni.
Baba wa marehemu, Musa Keya ameeleza kuwa waliposikia purukushani jikoni, walikimbia kwenda kuchunguza. Hata hivyo, Juma alikimbia mara walipofika eneo la tukio na Winnie alikutwa na majeraha makubwa ya kuchomwa kisu kichwani, usoni, kifuani, na tumboni.
Kwa mshangao, mwili wa Juma ulipatikana umbali wa mita chache kutoka nyumbani kwa familia ya Winnie na Polisi wanashuku kuwa Juma alikunywa sumu kabla ya kujikata shingo, hatua iliyosababisha kifo chake kutokana na kuvuja damu kupita kiasi.
Miili ya wanandoa hao imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Jumia, Vihiga, ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kina.