
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia Loveness Kisile (30) mkazi wa Mtaa wa Temeke, Kata ya Mhandu Wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa mume wake na ndugu zake kuwa ametekwa.
Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema tukio hilo limetokea Septemba 24, 2025, saa 5:30 usiku Mtaa wa Temeke ambapo mtuhumiwa alimpigia simu mume wake aitwaye Hosea Lusigwa na kumweleza kuwa ametekwa na watu watatu wa jinsi ya kiume, hivyo wanahitaji shilingi milioni 10 ili wasimdhuru na kuondoa ujauzito wake.
“Alidai kuwa ametekwa na watu watatu waliokuwa wakitumia usafiri wa pikipiki na gari ambazo namba zake za usajili hakuweza kuzitambua, akidai watu hao walimkamata kwa nguvu na kumvalisha mfuko wa sulphate usoni kwa lengo la kutowatambua, kisha kumpeleka kusikojulikana,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya muda, mtuhumiwa alimjulisha mume wake kuwa mimba yake imetolewa na kwamba watoto wake mapacha watatu wamefariki, na kusisitiza kuwa atumiwe kiasi hicho cha fedha ili aachiwe huru. Hata hivyo, taarifa hizo ziliripotiwa polisi na mume wa mtuhumiwa.
“Upelelezi kuhusu tukio hilo ulianza mara moja ambapo ilipofika majira ya saa 10:00 alfajiri ya Septemba 25, 2025 askari walifanikiwa kumkamata Loveness Kisile aliyekuwa anadai ametekwa akiwa salama na nguo zake akiwa amezichana yeye mwenyewe huko Mtaa wa Mecco, Kata ya Buzuruga Wilaya ya Ilemela,” imeeleza.
Jeshi la Polisi limesema baada ya mahojiano ya awali, mtuhumiwa alikiri kutoa taarifa za uongo, na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu amethibitika kuwa hakuwahi kupata ujauzito.
Aidha, baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa ameeleza kuwa alifanya hivyo ili mume wake na wakwe zake waendelee kumwamini na waweze kutoa mahari nyumbani kwao, na kwamba pesa hizo alizokuwa akidai zitumwe zilikuwa ni kwa manufaa yake mwenyewe.








