Amfungulia mashtaka mama mkwe kwa kumuunguza na uji wa moto

0
46

Adamu Mohammed mkazi wa Mtaa wa Zanzibari, Manispaa ya Musoma mkoani Mara ameiomba Jeshi la Polisi kumkamata mama mkwe wake, Zainab Ally kwa madai ya kummwagia uji wa moto uliomjeruhi usoni na kifuani.

Alidai kuwa tukio hilo lilitokea Machi 9 mwaka huu nyumbani kwa mama wa mke wake, Happiness Moses alipokwenda kumtembelea mwanae na mkewe ambao wote wanaishi nyumbani hapo baada ya kukorofishana.

Aidha, Mohammed ameeleza alikuwa akiwapelekea fedha za matumizi lakini mwishoni mwa Februari alishindwa kuendelea kuwahudumia kutokana na pikipiki aliyokuwa akiitumia kumuingizia kipato kuchukuliwa na mmiliki.

“Nimeshindwa kuwahudumia ndani ya wiki kama mbili hivi, mama mkwe na mke wangu walinishitaki Ustawi wa Jamii, nilijieleza ikaamriwa nijitahidi kwa chochote na mimi niliendelea kuwapelekea nilichokuwa napata,” alisema.

Siku ya tukio alikwenda nyumbani kwa mke wake pamoja na mke wa kaka yake wakitumia pikipiki ya rafiki yake kwenda kumchukua mtoto wake, ndipo mkwewe alichomoa ufunguo wa pikipiki na kumrushia mwanae ili aupeleke ndani.

Amesema baada ya hapo alimfuata mkewe ili kuchukua ufunguo huo na mara alipoupata ndipo mkwewe alipommwagia uji wa moto uliomjeruhi usoni na kufuani kwake.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longinus Tibishubwamu amethibitisha kuwapo kwa taarifa ya tukio hilo na kwamba jalada limepelekwa kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali.

Send this to a friend