
Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Musee Ngui, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake, Ngui Ngunza na kumzika kwenye shamba la familia yao kijijini Nguuni, Mwingi Magharibi nchini Kenya.
Maafisa wa Upelelezi wa Jinai (DCI) wameupata mwili wa mwanaume huyo katika Kaunti ya Kitui ambao ulizikwa kwa siri kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita huku mtuhumiwa akiwadanganya ndugu zake kuwa baba yake alisafiri, jambo lililozua wasiwasi kwa familia.
Mafanikio ya uchunguzi huo yamekuja baada ya Musee kukamatwa wiki mbili zilizopita eneo la Matuu, Kaunti ya Machakos alipokuwa amejificha. Kukamatwa kwake kulitokana na tuhuma tofauti za ubakaji na kuwapa mimba mabinti zake wawili.
Katika mahojiano, Musee alikiri kosa la mauaji na kuwaongoza maafisa hadi kwenye kaburi lililokuwa nyuma ya nyumba yao, na ndipo ufukuaji wa kaburi hilo ulifanyika na kukuta mabaki ya mwili huo.
Ndugu wa familia hiyo wameiomba serikali kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa ili haki iweze kutendeka.








