Amuua mpenzi wake anayedaiwa kuwa mwanafunzi na kujinyonga kisa wivu

0
2

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema linafanya uchunguzi kufuatia vifo vya watu wawili waliojulikana kwa majina ya Benadeta Silvester (21) mkazi wa Mtaa wa Makudi na Adam Kailanga (30) mfanyabiashara, vilivyotokea katika Mtaa wa Mkudi, wilayani Ilemela mkoani humo.

Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema Februari 4, 2025 jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo wakieleza kuonekana kwa miili ya watu hao katika chumba cha kupanga, ambapo askari walifika eneo hilo na kukuta mwili mmoja wa kike ukiwa sakafuni na wa kiume ukiwa unaning’inia juu ya paa la nyumba.

Polisi wamesema baada ya kuwahoji majirani walidai kulikuwa na ugomvi miongoni mwa watu hao ambao ni wapenzi baada ya mwanaume kumtuhumu mpenzi wake kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.

“Majirani walimsihi mwanaume huyo atulie kwakuwa migogoro ya kimapenzi ni mambo ya kawaida kwa watu wengi, ndipo mwanaume huyo alirudi ndani na hakutoka tena hadi majirani walipofungua mlango na kuwakuta wapenzi hao wakiwa wamefariki dunia,” imeeleza taarifa.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema uchunguzi umefayika na kubaini kuwa Benadeta alifariki baada ya kukabwa koo, na Adam kifo chake kilisababishwa na kujinyonga kwa kutumia mtandio.

Jeshi hilo limesema zipo taarifa kuwa Benadeta ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari Korogwe iliyopo mkoa wa Tanga na kwamba ufuatiliaji wa taarifa hizo unaendelea.

Send this to a friend