
Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 kutoka jiji la Dnipro, Ukraine, amehukumiwa kifungo cha miaka nane jela baada ya kupatikana na hatia ya usafirishaji haramu wa binadamu dhidi ya mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili.
Mahakama imetoa hukumu hiyo baada ya ushahidi kuonesha kuwa mama huyo, ambaye jina lake halijatajwa, alijaribu kumuuza mtoto wake wa kiume kwa pauni 18,000 [TZS milioni 64.5] akieleza kuwa alihitaji fedha hizo kuanzisha biashara yake binafsi.
Katika video iliyosambaa mtandaoni, afisa wa polisi ameonekana akihesabu fedha zilizotolewa na mnunuzi wakati mama huyo akifungwa pingu.
Aidha, mtaalamu wa ustawi wa jamii ameonekana akimbeba mtoto huyo na kumpeleka kwenye gari lililokuwa tayari kumchukua kwa ajili ya kumpeleka katika kituo cha kulelea watoto.
Polisi nchini Ukraine walimkamata mama huyo mara tu baada ya kupokea fedha taslimu kutoka kwa mtu aliyedaiwa kuwa mnunuzi, ambaye alikana madai yake mahakamani.
Uhalifu huo ulirekodiwa na idara ya uhamiaji ya polisi pamoja na kitengo cha upelelezi cha Idara Kuu ya Polisi katika mkoa wa Dnipropetrovsk kwa kushirikiana na idara ya uchambuzi wa kihalifu.