Angola: 50 wafariki kwa kunyweshwa mitishamba ili kujua kama ni wachawi

0
103

Watu zaidi ya 50 wamefariki nchini Angola baada ya kulazimishwa kunywa dawa ya mitishamba ili kuthibitisha kwamba hawakuwa wachawi.

Msemaji wa polisi, Antonio Hossi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika akieleza kwamba ni desturi inayojulikana sana katika jamii hiyo kuwalazimisha watu kunywa dawa hiyo kwa sababu ya imani potofu ya uchawi.

“Zaidi ya waathirika 50 walilazimika kunywa maji hayo ya ajabu ambayo kwa mujibu wa waganga wa kienyeji, yanathibitisha iwapo mtu anafanya uchawi au la,” amesema huku akiongeza kuwa kesi za namna hiyo zimekuwa zikiongezeka.

Angola ambayo haina sheria dhidi ya uchawi, imeiachia jamii kushughulika na suala hilo kama watakavyo, ambapo madai yanayohusu uchawi mara nyingi hupatiwa ufumbuzi na waganga wa jadi, ambao huwataka washukiwa kunywa kinywaji cha mitishamba kinachoitwa ‘Mbulungo’ ambacho kinaaminika kuwa endapo mtu atafariki baada ya kunywa kinywaji hicho, basi alikuwa ni mchawi.

Mwaka jana, mmoja wa kiongozi wa dini nchini humo alisema kwamba changamoto za kijamii na kiuchumi nchini humo zinawalazimu baadhi ya watu kujihusisha na uchawi kwa sababu wanaamini kuwa, kwa uchawi wanaweza kupata kile wanachotaka na hivyo kujikomboa kutoka kwenye umaskini na kupata kila kitu wanachohitaji ili kuishi.

Send this to a friend