Apandishwa kizimbani kwa kosa la kumshambulia mke wake

0
39

Hamza Omary (38), fundi selemala na mkazi wa Luchelele amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo ya Mkuyuni, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza akikabiliwa na shtaka la kumshambulia mke wake, Anna Zacharia.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 07, 2026 saa 3.30 usiku, ambapo alimshambulia mke wake kwa kumpiga ngumi, kumrushia sufuria kichwani na kumng’ata mkono wa kushoto.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, Witness Ndosi, Mwendesha Mashtaka Koplo Dorothy Mauma amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 240 cha Sura ya 16 ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Marejeo ya mwaka 2023.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana shtaka hilo na amepelekwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.

Masharti ya dhamana yalikuwa ni kuwa na mdhamini mmoja, barua ya utambulisho kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kata pamoja na fungu la dhamana la ahadi kiasi cha shilingi laki moja. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 02, 2026.

Send this to a friend