Apatikana na hatia ya mauaji ya jirani yake aliyemkuta chini ya kitanda

0
87

Mwanaume mmoja huko Nakuru nchini Kenya aitwaye Cyrus Kipng’eno Rono amepatikana na hatia ya mauaji baada ya kumshambulia jirani yake aitwaye Moody Awori aliyemkuta amejificha chini ya kitanda chake akiwa nusu uchi.

Jaji Samuel Mohochi amehitimisha kesi hiyo iliyochukua takriban miaka miwili kwa kusema kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa Rono ndiye aliyemuua jirani yake Awori aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo na mke wa mshitakiwa.

Tukio hilo lilitokea Agosti 29, 2023, wakati Rono akiwa kwenye kazi yake ya ulinzi usiku eneo la Kiamunyeki ambapo alijaribu kumpigia mke wake simu bila mafanikio na baadaye aliondoka kazini na kurejea nyumbani majira ya saa 3 usiku.

Kwa mujibu wa maelezo ya mshitakiwa, baada ya kufika nyumbani aligonga mlango wa chumba chake lakini mkewe alichelewa kufungua, na alipotoka alionekana mwenye wasiwasi. Rono aliendelea kuchunguza chumbani na ndipo alipomkuta Awori akiwa nusu uchi, amejificha chini ya kitanda.

Mshitakiwa alichukua panga na kumshambulia, akimkata shingoni na mikononi kisha baada ya tukio hilo, Rono alienda Kituo cha Polisi Lanet kuripoti na kisha akawaongoza askari hadi eneo la tukio ambapo alikamatwa.

Ripoti ya Daktari wa Uchunguzi wa Serikali, Titus Ngulungu, ilionesha kuwa Awori alifariki kutokana na majeraha makubwa ya kichwa yaliyosababishwa na kupigwa kwa nguvu na kukatwa kwa kutumia silaha kali.

Send this to a friend