Baada ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutangaza kuanza matumizi ya kitita kipya cha mafao kitakachoanza Machi Mosi, 2024, Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania (APHFTA) vimesema vituo vyao vitashindwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kupitia kitita hicho kutokana na kutoendana na uhalisia wa soko.
Kupitia taarifa kwa umma ya APHFTA iliyosainiwa na mwenyekiti wake wa taifa, Dkt. Egina Makwabe imesema mazungumzo yao na kamati maalum ya Serikali iliyoundwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu yameshindwa kupata muafaka, hivyo wanachama wa NHIF wanaombwa kuwasiliana na mfuko ili kujua namna ya kupata huduma hizo.
“Kama kitita kipya cha NHIF cha bei za huduma ya afya kilichopendekezwa na kamati teule ya waziri kitatangazwa kuanza kutumika, itakuwa kinyume cha mapendekezo ya bunge ya kumalizwa tatizo hili kwa maridhiano,” imeeleza taarifa.
Januari 4 mwaka huu Waziri Ummy alikutana kwa ajili ya mazungumzo na APHFTA. Baada ya mazungumzo, Serikali ilisitisha bei mpya za kitita cha matibabu zilizowekwa na NHIF na waziri kutangaza kuunda kamati huru itakayofanya mapitio ya maboresho yaliyofanyika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Mwananchi, mmoja wa maofisa waandamizi wa APHFTA amesema wamefikia uamuzi huo kutokana na bei kwenye kitita hicho kushuka kwa kati ya asilimia 20 hadi 30, wakati thamani ya Dola ya Marekani, dawa zikiwa zimepanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema milango iko wazi kwa APHFTA ili kupokea maoni yao na kuwahakikishia wanachama kuwa hakuna ambaye atakosa huduma ya matibabu.