Arusha: Kijiji chapiga marufuku suruali za kubana, vimini na viduku

0
41

Uongozi wa Kijiji cha Olevolosi, Kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha umepiga marufuku kwa wasichana na wanawake kuvaa suruali za kubana na sketi fupi vinginevyo watajibika kulipa faini ya shilingi 50,000.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa kijiji hicho, Mtendaji wa Kata hiyo ya Kimnyak, Joshua Mollel, amewasilisha sheria hizo kwa niaba ya mtendaji wa kijiji hicho ambazo zimepitishwa na mkutano huo kama sheria ndogo.

“Marufuku kwa msichana au mwanamke yoyote kuvaa suruali ya kubana na kuonyesha maungo yake au kimini ukibainika faini yake ni shilingi 50,000, na kama hauna hapo kuna akina mama walioandaliwa tumeambiwa tuwaletee,” amesema.

Aidha, uongozi umepiga marufuku kwa vijana wa kiume kusuka nywele au kunyoa pembezoni mwa kichwa na kuacha katikati ‘kiduku’ au kuvaa suruali mlegezo inayoonyesha makalio au iliyotobolewa, na kwamba endapo kijana yeyote atakiuka marufuku hiyo atatakiwa kulipa faini yake ya shilingi 50,000.

Sheria nyingine zilizowekwa ni pamoja na kijana wa kiume kuvalia hereni na vijana wenye nguvu kukaa kijiweni asubuhi bila kufanya kazi ambao pia watatozwa faini shilingi 50,000.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend