Asahi Group kununua hisa za Diageo katika EABL

Asahi Group kununua hisa za Diageo katika EABLNairobi, Desemba 17, 2025: Kampuni ya East African Breweries PLC (EABL) imetangaza kuwa kampuni ya Diageo imekubali kuuza hisa zake zote za EABL na umiliki wake katika kampuni ya vinywaji vikali ya UDV (Kenya) Limited kwa kampuni ya Asahi Group kutoka Japan.
Hatua hii inaifanya Asahi kuwa kampuni ya kwanza kubwa kutoka Japan kuingia rasmi na kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika biashara ya vinywaji barani Afrika.
Baada ya ununuzi huu kukamilika, Asahi itakuwa mmiliki mkuu wa EABL na itasimamia shughuli zake zote nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kuziendeleza chapa za ndani ambazo wananchi wamezizoea, huku pia ikileta baadhi ya chapa zake maarufu duniani kwa walaji wa Afrika Mashariki.
Kwa makubaliano haya, Diageo inatarajia kupata mapato ya takribani dola bilioni 2.3 za Marekani baada ya kodi na gharama nyingine, sawa na shilingi Trilioni 5.69 za Tanzania. Thamani ya jumla ya EABL kwa makubaliano haya imekadiriwa kufikia dola bilioni 4.8, sawa na takribani Shilingi trilioni 11.87 za Tanzania .Ununuzi huu unaonesha imani kubwa ya wawekezaji katika ukuaji wa EABL na mustakabali wa soko la Afrika Mashariki, eneo ambalo linaendelea kukua kwa kasi kiuchumi na kwa idadi ya watu. Chini ya umiliki mpya, EABL inatarajiwa kuendelea kufanya vizuri na kupanua biashara yake zaidi.
EABL imeeleza kuwa inaingia katika ukurasa mpya wa ukuaji pamoja na Asahi, kampuni ambayo itanufaika na viwanda vya kisasa vya EABL, uzoefu wa uongozi wake, chapa imara, mtandao mzuri wa usambazaji pamoja na mahusiano mazuri na wafanyakazi, washirika na wateja.Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa EABL, Bi. Jane Karuku, alisema kuwa ununuzi huo ni fursa kubwa kwa kampuni.
Alisema mmiliki mpya analeta uzoefu mkubwa wa kimataifa katika ubunifu na ukuzaji wa chapa, jambo litakalosaidia EABL kufikia lengo lake la kuwa kampuni ya vinywaji inayoheshimika zaidi barani Afrika.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa mpito wa Diageo, Bw. Nik Jhangiani, alisema Diageo inajivunia safari na mafanikio ya EABL katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania. Aliongeza kuwa Diageo itaendelea kushirikiana na Asahi kupitia matumizi ya baadhi ya chapa zake katika eneo la Afrika Mashariki, huku muamala huu ukiisaidia Diageo kuimarisha hali yake ya kifedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Asahi Group, Bw. Atsushi Katsuki, alisema EABL ni kampuni imara yenye nafasi kubwa sokoni, ikiwa na chapa zenye nguvu, viwanda vya kisasa na timu yenye uzoefu. Alisema Asahi inalenga kukuza biashara kwa njia endelevu na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi zinazohusika.
Muamala huu bado unahitaji kibali kutoka kwa mamlaka za serikali na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026. EABL imesisitiza kuwa hakutakuwa na mabadiliko katika shughuli zake za kila siku na hakuna wafanyakazi watakaopoteza ajira kutokana na mabadiliko haya.Katika kipindi cha mpito, Diageo itaendelea kushirikiana na Asahi ili kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kwa utulivu na shughuli zinaendelea bila usumbufu.
MwishoKwa Mawasiliano Zaidi Wasiliana na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha EABL kwa Simu namba: Eric Kiniti +254722855514David Kimondo +254721610103Na Tanzania wasiliana na:Rispa Hatibu0685260901Taarifa kwa Wahariri wa HabariKuhusu EABLEast African Breweries PLC (EABL) ni moja ya makampuni makubwa na yanayoongoza katika biashara ya vinywaji vyenye kilevi Afrika Mashariki.
Kampuni hii inazalisha na kusambaza aina mbalimbali za bia na vinywaji vikali vinavyopendwa na walaji.Shughuli kuu za EABL zipo nchini Kenya, Uganda na Tanzania, lakini bidhaa zake zinapatikana pia katika nchi zaidi ya 10 barani Afrika na maeneo mengine duniani. Chapa zake zinajumuisha mchanganyiko wa bidhaa za asili za Afrika Mashariki pamoja na chapa za kimataifa zinazotambulika kwa ubora wa hali ya juu. Baadhi ya chapa hizo ni Tusker, Guinness, Bell Lager, Serengeti Lager, Kenya Cane, Chrome Vodka, Johnnie Walker, Captain Morgan na Smirnoff.Lengo la EABL ni kuwa miongoni mwa makampuni bora zaidi ya bidhaa za matumizi barani Afrika, yanayoaminika na kuheshimiwa na jamii. Kampuni inajivunia chapa zake na furaha inayowaletea mamilioni ya watu, huku ikisisitiza matumizi yenye uwajibikaji wa pombe kama sehemu ya maisha yenye uwiano.
Kuhusu DiageoDiageo ni kampuni kubwa ya kimataifa inayojihusisha na biashara ya vinywaji vyenye kilevi, ikimiliki mkusanyiko mpana wa chapa maarufu za bia na vinywaji vikali duniani. Chapa zake ni pamoja na Johnnie Walker, Crown Royal, J&B, Buchanan’s, Smirnoff, Ketel One, Captain Morgan, Baileys, Don Julio, Tanqueray na Guinness.Bidhaa za Diageo zinauzwa katika karibu nchi 180 duniani. Kampuni hii imeorodheshwa katika masoko ya hisa ya London na New York.
Diageo pia inaendesha kampeni na programu mbalimbali zinazohamasisha unywaji wa pombe kwa uwajibikaji.Kuhusu AsahiAsahi ni kampuni kubwa ya kimataifa inayozalisha na kusambaza vinywaji mbalimbali, ikijumuisha bia, vinywaji vyenye na visivyo na kilevi, pamoja na bidhaa za chakula. Lengo lake ni kuleta ladha bora na kuongeza furaha katika maisha ya watu.Asahi ilianzishwa nchini Japan mwaka 1889 na tangu wakati huo imekuwa ikijikita katika ubunifu na ubora. Kupitia safari yake ya zaidi ya karne moja, Asahi imekusanya chapa maarufu na uzoefu kutoka kwa viwanda vya bia vinavyotambulika duniani, vingi vikiwa na historia ndefu.Chapa zake maarufu ni pamoja na Asahi Super Dry, Peroni Nastro Azzurro, Kozel, Pilsner Urquell na Grolsch. Kauli mbiu ya Asahi, “Make the world shine”, inaonesha dhamira ya kampuni ya kuunganisha watu na kuchangia kujenga dunia yenye mustakabali endelevu.Asahi ina shughuli zake katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Japan, Asia ya Mashariki, Ulaya na Asia Pacific. Kila mwaka, kampuni husambaza zaidi ya lita bilioni 10 za vinywaji duniani na kupata mapato ya zaidi ya yen trilioni 2.9 za Japan. Makao makuu ya Asahi yapo Japan na kampuni imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Tokyo.









