Ashikiliwa kwa kumwagia maji ya moto mke mwenzake msibani

0
14

Mkazi wa Kata ya Lugata, Kisiwa cha Kome wilayani Sengerema, Vumilia Kasembo (32) anashikiliwa na Ofisi ya Mtendaji wa Kata kwa madai ya kumwagia maji ya moto mke mwenzake Mariam Paul (30), baada ya kukutana kwenye msiba wa baba mkwe wao.

Ofisa Mtendaji Kata ya Lugata, Rafael Jangol, amesema baada ya kumhoji mtuhumiwa amekiri kufanya kosa hilo huku akidai kuwa ni wivu wa mapenzi uliopelekea kufanya jambo hilo baada ya kumwona mke mwenzake.

“Tunamshiria kwa sasa huku tukiandaa taratibu za kumpeleka polisi kwa ajili ya taratibu zingine, Mariamu Paul ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake huku mkono wa kushoto ukiwa umeungua zaidi,” amesema Jangole.

Akielezea tukio, Mariamu amesema alitoka nyumbani kwake Kijiji cha Bukokwa na kuelekea Kijiji cha Lugata kwa ajili ya msiba wa baba mkwe wake, na kwamba baada ya maziko kumalizika, muda wa saa 2:00 usiku alikwenda kulala, na hapo ndipo alipomwagiwa maji ya moto na kukimbia.

Kwa upande wake, Ndagabwene Evalist (33), ambaye ndiye mume wa wawili hao, amesema anashangwazwa na kitendo hicho kilicholeta fedheha kwa jamii, kwani tayari alikuwa ameshamjulisha mke mkubwa (Vumilia), kuwa ana mke mwingine ambaye anaishi Kijiji cha Bukokwa, lakini walikuwa hawajawahi kuonana.

Akizungumza mtuhumiwa wa tukio hilo, Vumilia amesema kilichomtuma kufanya hivyo ni hasira baada ya kumwona mke mwenzie akiwa msibani hapo ambaye alikuwa hajawahi kukutana naye wala kitambulishwa rasmi na mume wake.
Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend