Ashikiliwa kwa kutoa taarifa za uongo za wizi ili apewe malipo ya bima

0
1

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linamshikilia David Zefania Sanga (39) mfanyakazi wa zamani wa kampuni ya Bima ya UAP kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo polisi kuhusu wizi wa vifaa vya magari.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema mtuhumiwa huyo alitoa taarifa hiyo katika kituo cha polisi Kigamboni kuwa magari mawili namba T 811 DUL Toyota Crown na T. 647 DRE Mitsubishi Outlander vifaa vyake mbalimbali vimeibiwa, na baada ya uchunguzi polisi walibaini kuwa mtuhumiwa aliving’oa na kuvificha nyumbani kwake ili kujipatia fedha kwenye kampuni ya bima.

“Vifaa vilivyong’olewa na kufichwa ni bampa za mbele na nyuma, window covers, redio za gari, side mirrors, taa zote za mbele na nyuma, power windows na betri. Hatua za kisheria za haraka dhidi ya mhusika zinakamilishwa ili afikishwe kwenye vyombo vingine vya kisheria,” imesema taarifa.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linakemea vikali tabia za kutoa taarifa za uongo kwa makusudi kwa maafisa wa serikali, na kwamba halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo.

Send this to a friend