
Jeshi la Polisi mkoani Mara linamshikilia Nyabusa Musa Daudi (31) kwa tuhuma za mauaji ya Ibrahim Wambura Daudi (05) mkazi wa kijiji cha Kemgesi Wilaya ya Serengeti mkoani humo.
Mtoto huyo aliuawa Septemba 19, 2025 kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mtuhumiwa ambaye ni mtoto wa baba yake mkubwa, majira ya saa 12:00 jioni wakati ambapo wazazi wa marehemu wakiwa nje ya nyumba hiyo.
“Wakati wa tukio hilo, baba na mama wa marehemu walikuwa kwenye sherehe ya harusi kijiji cha jirani na nyumbani, walimuacha marehemu akiwa na kaka yalr mwenye umri wa miaka 8, pamoja na mtuhumiwa,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Imeongeza kuwa “Wakiwa ndani mtuhumiwa alifunga mlango wa nyumba na kutekeleza mauaji hayo na pindi tukio likiendelea, kaka wa marehemu alifanikiwa kutoroka kupitia dirishani na kuanza kupiga kelele akiomba msaada kwa majirani. Baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia.”
Aidha, Jeshi la Polisi limesema kwa kushirikiana na wananchi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa amejificha katika Kijiji cha Jitununu. Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.








