Ashikiliwa kwa tuhuma za kuchoma nyumba iliyoua watu tisa, chanzo mgogoro wa ardhi

0
2

Jeshi la Polisi nchini Kenya linamshikilia Christopher Okello Owino kama mshukiwa mkuu wa tukio la kuchoma nyumba moto uliosababisha vifo vya watu tisa wa familia moja usiku wa Jumanne huko Sigomere, Kaunti Ndogo ya Ugunja.

Kikosi cha usalama kutoka Kaunti ya Siaya kilisafiri usiku kucha hadi Nairobi kumchukua mshukiwa ambaye amekamatwa nyumbani kwake eneo la Kianda, Kibra, na maafisa wa upelelezi wa eneo hilo.

Baada ya kukamatwa, vikosi vya usalama kutoka Siaya na Kibra vililinganisha taarifa zao za kipelelezi na kuthibitisha kuwa Owino ndiye mshukiwa wa shambulio hilo la moto.

Timu ya DCI kutoka Ugunja iliwasili Nairobi wakiwa na mke wa Owino, ambaye alikamatwa mapema Jumatano baada ya polisi kukuta mtungi wa petroli unaoshukiwa kutumika kuchoma nyumba hiyo, nyumbani kwao katika kijiji cha Upanda, Sigomere.

Owino anadaiwa kupanga moto huo mbaya ulioteketeza familia nzima, kwa madai kuwa ulikuwa ni matokeo ya mgogoro wa ardhi kijijini humo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kibra, Patricia Yegon, amethibitisha kukamatwa kwa mshukiwa na kusema kwamba atakabidhiwa kwa mamlaka za Siaya kwa uchunguzi zaidi na mashitaka.

Send this to a friend