Ashikiliwa kwa tuhuma za kumnyonga mtoto wa miaka saba

0
85

Mwanaume mmoja mkazi wa Kijiji cha Mahango wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumfanyia ukatili, udhalilishaji na kumuua kwa kumnyonga mtoto wa miaka saba, Amedeus Laurent kisha mwili wake kuuficha kwenye shamba la migomba.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa imesema mama mzazi wa mtoto huyo alifika kituo cha Polisi Agosti 6, 2024 kutoa taarifa kuwa mtoto wake haonekani tangu Agosti 5 saa 12.00 jioni, na baada ya uchunguzi kufanyika, mtuhumiwa alionekana akiwa na mtoto huyo.

“Kutokana na taarifa hiyo mtuhumiwa alikamatwa lakini alipoulizwa alikana hakuwahi kuwa karibu na mtoto huyo,” amesema Kamanda Maigwa.

Ameongeza kuwa jeshi la polisi liliendelea kumhoji mtuhumiwa, na hadi kufikia Agosti 9, 2024 Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliupata mwili wa mtoto huyo ambapo baada ya mwili kuonekana, mtuhumiwa alikiri kufanya uhalifu huo.

Kamanda Maigwa ameeleza kuwa Jeshi linaendelea kukamilisha taratibu za kiuchunguzi ili mtuhumiwa huyo aweze kufikishwa mahakamani.

Send this to a friend