Ashikiliwa kwa tuhuma za kumuua kichanga baada ya kuzidiwa majukumu

0
7

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linamshikilia mwanamke aliyefahamika kwa jina la Zulpha Mathew Timamu (26) mkazi wa Kata ya Tandika wilayani Mtwara kwa tuhuma za mauaji ya kichanga chenye jinsia ya kiume muda mchache baada ya kujifungua.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema tukio hilo limetokea Juni 02, 2025 saa tisa alasiri nyumbani kwa mtuhumiw,a baada ya majirani kusikia sauti ya mtoto mchanga akilia kisha baada ya muda mfupi, sauti hiyo haikusikika tena, hali iliyowapa wasiwasi na kuamua kutoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara.

“Chanzo cha tukio hilo ni baada ya mtuhumiwa kuona atazidiwa na majukumu ya kulea mtoto, kwakuwa kabla ya kichanga hicho kuzaliwa mtuhumiwa alikuwa ana mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu ambaye bado ananyonya,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, imesema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa alijifungua salama na baada ya kujifungua alimchukua mtoto huyo na kumweka kwenye ndoo ndogo yenye ujazo wa lita 10, kisha kufunika ndoo hiyo na mfuniko, kitendo kilichopelekea kichanga hicho kukosa hewa na kupoteza maisha.

Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Send this to a friend